
Uzalishaji na Usambazaji wa Miche ya Kahawa
Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa, inaratibu uzalishaji na usambazaji wa miche bora ya kahawa katika maeneo yote ya uzalishaji nchini. Zoezi hili lina lengo la kuhakikisha wakulima wanapata miche yenye ubora wa juu inayostahimili magonjwa, sambamba na kuongeza tija na ubora wa kahawa ya Tanzania katika soko la ndani na la kimataifa.
Uzalishaji wa Miche
- Miche huzalishwa kupitia vitalu vya umma vinavyosimamiwa na TCB, Taasisi, makampuni,vitalu vya watu binafsi na vya vikundi vya wakulima.
- Mbegu bora zinazotolewa na TaCRI hutumika ili kuhakikisha miche inayozalishwa inakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Usambazaji wa Miche
- Usambazaji wa miche hufanyika katika kanda zote zinazolima kahawa, kwa kuzingatia msimu wa mvua. Kwa kawaida, zoezi hili huanza mwezi Oktoba hadi Machi, kulingana na mwenendo wa mvua katika kila eneo.
- Wakilima hupatiwa miche kupitia halmashauri zao kwa uratibu wa vyama vya ushirika (AMCOS) na viongozi wa kilimo katika ngazi za wilaya.
- Serikali, kupitia TCB na wadau wa maendeleo, imekuwa ikisaidia kugawa miche kwa ruzuku au bure ili kuongeza wigo wa upandaji wa kahawa na kuanzisha mashamba mapya.
Umuhimu wa Zoezi Hili
- Kuwezesha upatikanaji wa miche bora kwa wakulima wadogo na wakubwa.
- Kuongeza mavuno na ubora wa kahawa ya Tanzania, hivyo kuongeza kipato cha kaya na pato la taifa.
- Kuhamasisha vijana na vikundi vya wanawake kushiriki katika kilimo cha kahawa kupitia upandaji wa mashamba mapya.
- Kuweka msingi wa ukuaji endelevu wa sekta ya kahawa nchini.