JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KILIMO
BODI YA KAHAWA TANZANIA
TANGAZO
UFUNGUZI WA MSIMU WA KAHAWA 2024/ 2025
Utangulizi
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania anawatangazia ufunguzi wa msimu mpya wa ununuzi wa kahawa kwa mwaka 2024/2025. Tangazo hili linatolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 23 (1) ya Kanuni za Kahawa 2013. Tarehe za ufunguzi wa msimu na kuanza kwa ununuzi wa kahawa katika kanda za uzalishaji kahawa ni kama ifuatavyo;
Na. |
Kanda |
Mkoa |
Tarehe ya Ufunguzi |
1. |
Kigoma |
Kigoma, Katavi |
1 Mei, 2024 |
2. |
Mara |
Mara, Mwanza |
20 Aprili, 2024 |
3. |
Kagera |
Kagera |
1 Mei, 2024 |
4. |
Mbeya, Songwe |
Mbeya, Songwe |
15 Juni, 2024 |
5. |
Ruvuma |
Ruvuma, Iringa, Njombe |
1 Julai, 2024 |
6. |
Kaskazini |
Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Morogoro, Tanga |
1 Julai, 2024 |
Mambo muhimu ya kuzingatia katika msimu huu 2024/2025
- Bodi inawashauri wafanyabiashara wa kahawa kuwasilisha maombi yao ya leseni mapema na kuzingatia kanuni ya 35 (1) na (2) ya kanuni za Tasnia ya Kahawa 2013 wakati wa maombi ya leseni zao. (Prohibition of multiple licenses regulation). Kwa mujibu wa kanuni hii kampuni moja haitapewa leseni zifuatazo kwa wakati mmoja; Leseni ya kununua kahawa (Coffee buying license), Leseni ya viwanda vya kukoboa kahawa (Coffee curing lisence) au leseni ya kusafirisha kahawa nje ya nchi (Green coffee export licence). Mdau mwenye nia ya kuendeleza ubora wa kahawa yake kwa ajili ya soko maalum anaweza kupewa leseni ya kununua kahawa na leseni ya kiwanda cha kukobolea kahawa na ataruhusiwa kukoboa kahawa yake tu.
- Bodi inatoa taarifa kuwa kuanzia msimu huu wa kahawa 2024/2025 Bodi itaanza kuendesha minada ya kahawa ghafi za arabika laini (Arabica Parchment Coffee). Taratibu za uendeshaji wa minada hii zitatolewa kwenye mwongozo wa masoko utakaotolewa na Bodi kwa mujibu wa sheria.
- Bodi inashauri Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya zinazolima kahawa kutoa vibali vya kununua kahawa kwa wanunuzi binafsi watakaoomba kununua kahawa kwenye Halmashauri zao mapema kabla ya tarehe ya kuanza msimu ikiwa ni moja ya masharti yaliyotolewa ili kupata leseni ya ununuzi wa kahawa kwa mujibu wa Jedwali la Tatu la Kanuni za Kahawa 2013. Endapo Halmashauri itachelewesha au kukataa kutoa kibali pasipo sababu za msingi, Bodi itatoa leseni kwa mujibu wa Kanuni ya 26 (2) ya Kanuni za Kahawa, 2013.
- Maombi ya leseni zote mpya na maombi ya kuhuisha (renewal) leseni kwa wanunuzi binafsi yatafanyika kwa njia ya mtandao katika mfumo wa ATMIS kwa kufuata kiungo cha https://atmis.kilimo.go.tz.
- Vyama vyote vya msingi vinatakiwa kuanza kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima na kuitayarisha kwa ajili ya kuuzwa katika masoko ya kahawa mara tu inapokuwa tayari ili kuwezesha kahawa hiyo kuuzwa na wakulima kulipwa fedha zao mapema.
- Bodi ya Kahawa Tanzania itaanza kuendesha minada ya kahawa ghafi Kagera mara tu itakapopokea taarifa za uwepo wa kiasi cha kutosha cha kahawa kuendesha mnada kutoka kwenye Vyama vya Ushirika vya Msingi. Pia Bodi itaanza kuendesha minada ya kahawa safi baada ya kupokea taarifa za uwepo wa kahawa na sampuli kutoka viwanda vya kukobolea kahawa.
- Vyama vyote vya Msingi vya Ushirika katika Mkoa wa Kagera vinaelekezwa kuhakikisha kuwa vinatumia mizani zilizohakikiwa wakati wa mapokezi ya kahawa za wakulima. Vyama Vikuu vinaelekezwa kuhakikisha kuwa mizani hizo zimekaguliwa na kuwa zinafanya kazi kabla ya tarehe ya kuanza kwa msimu.
- Vyama vya Ushirika vya Msingi vitapaswa kuhakikisha kuwa akaunti zao za malipo zipo hai (zinafanya kazi) ili kuwezesha zoezi la uuzaji wa kahawa na malipo kufanyika mapema na kuepuka ucheleweshwaji wa malipo ya fedha za wakulima.
- Vyama vya Ushirika vya Msingi vitakavyouza kahawa mnadani vitahuisha vibali vyao au kuomba vibali vipya kwa kujaza fomu maalum. Fomu hizo zinapatikana katika tovuti ya Bodi ya Kahawa, ofisi za Kanda za Bodi ya Kahawa, viwanda vya kukobolea kahawa na ofisi za Vyama Vikuu vya Ushirika. Pale itakapobidi Vyama hivi vitasaidiwa kuomba vibali katika mfumo wa ATMIS na maofisa waliopo kwenye ofisi za kanda za Bodi ya Kahawa, Viwanda vya kukobolea kahawa na Vyama Vikuu vya Ushirika.
- Vyama vya Ushirika vya Msingi vikamilishe mapema taratibu za upatikanaji wa mitaji ili vianze ukusanyaji wa kahawa ya wakulima wao mara tu kahawa inapokuwa tayari.
- Vyama vya Ushirika vihakikishe kuwa mitambo ya kuchakata kahawa (CPU) iliyoko katika maeneo yao inatumika na inafunguliwa mara tu kahawa inapokuwa tayari ili kufanikisha lengo la Serikali la kuongeza ubora wa kahawa na bei ya mkulima.
- Makampuni binafsi yaliyoingia makubaliano ya kilimo cha mkataba na Vyama vya Ushirika wanatakiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa makubaliano yao kwa ajili ya tathimini na ufuatiliaji kwa mujibu wa Kanuni ya 59 ya Kanuni za Tasnia ya Kahawa 2013 kabla ya makubaliano ya mauziano ya kahawa kufanyika. Bodi haitasajili makubaliano ya kilimo cha mkataba wakati wa mauzo ya kahawa.
- Utaratibu wa ukusanyaji, uuzaji na ununuzi wa kahawa ghafi (Dry Cherry) kupitia Vyama vya Msingi na pia uendeshaji wa minada ya kahawa ghafi katika Mkoa wa Kagera utafanyika kama ilivyofafanuliwa katika Mwongozo Na. 1 wa Usimamizi wa Masoko na Mauzo ya Kahawa kwa Msimu 2023/2024.
Primus O. Kimaryo
Mkurugenzi Mkuu
Bodi ya Kahawa Tanzania
S. L. P. 732 – Moshi, Simu: 027-2752324
Barua pepe: info@coffee.go.tz; Tovuti: www.coffee.go.tz