Imewekwa: 19 Sep, 2025
Mabalozi wa Umoja wa Ulaya Watembelea Bodi ya Kahawa Tanzania

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imepokea ugeni wa Mabalozi 12 kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), waliotembelea Makao Makuu ya Bodi mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, kama sehemu ya ziara yao ya kikazi ya siku tatu Mkoani Kilimanjaro kuanzia Septemba 17–19, 2025.

Katika ziara hiyo, mabalozi hao walikutana na menejimenti ya TCB ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Primus Kimaryo, pamoja na wawakilishi wa taasisi za utafiti na waratibu wa miradi ya maendeleo ya kahawa ikiwemo Mradi wa EU Deforestation Regulation (EUDR).

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bw. Kimaryo aliwakaribisha mabalozi hao na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya katika kukuza tasnia ya kahawa. Aliwaomba kuendelea kuwa washirika wakuu katika kuoanisha uwekezaji, kushiriki utaalamu wa kiufundi na kufadhili miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa EUDR, Bw. John Mabagala kutoka taasisi ya Emergency Marketing International (EMI), aliwasilisha maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya. Alifafanua kuwa mradi huo unalenga kusaidia sekta ya kahawa nchini kukidhi vigezo vya sheria mpya ya EU kuhusu ulinzi wa mazingira.

“Kwa sasa, taarifa za wakulima wa kahawa zimeanza kukusanywa mkoani Kagera na Songwe ili kuunda kanzi data ya kitaifa ya wakulima wa kahawa itakayokuwa chini ya usimamizi wa Bodi ya Kahawa,” alisema Bw. Mabagala.

Mabalozi hao walieleza kufurahishwa na maendeleo ya sekta ya kahawa nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa msaada na ufadhili wa miradi mbalimbali ya kukuza tasnia hiyo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Bi. Christine Grau, alisema ziara hiyo ni kielelezo cha ushirikiano wa muda mrefu kati ya EU na Tanzania, hususan katika kipindi hiki ambacho kinadokeza maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano wa EU–Tanzania na miaka 25 ya ushirikiano wa EU–AU.

“Ziara hii ni nafasi ya kipekee kuona matokeo chanya ambayo miradi yetu inaleta kwa wakulima, wajasiriamali wa kilimo na taasisi za ndani. Pia inatupa nafasi ya kusikiliza moja kwa moja kutoka kwa wale wanaoleta mabadiliko. Lengo letu ni kuimarisha uzalishaji, uendelevu na ustahimilivu wa sekta ya kahawa tukijenga juu ya uhusiano wa muda mrefu kati ya EU na Tanzania,” alisema Bi. Grau.

Mabalozi wa EU waliokuwa sehemu ya ziara hiyo wanatoka nchi za Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Hispania na Uswidi