
Tarehe 3 Julai, 2025
"SIKU YA UFUNGUZI"
Wadau wa Tasnia ya kahawa wamekutana tarehe 3 Julai,2025 katika kongamano la wadau wa kahawa kwa mwaka 2025 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper jijini Dodoma, na kujadili masuala mbali kuhusu Taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo ya Kahawa kwa mwaka 2021-2025, Maendeleo ya Sekta ya Kahawa katika Kutekeleza Matakwa ya Sheria ya Kuzuia Uharibifu wa Misitu la Jumuiya ya Ulaya (EUDR).
Akijibu maswali kuhusu hoja mbali mbali kutoka kwa wadau kuhusu mada zilizowasilishwa, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Bw. Primus Kimaryo amesema, Serikali inaendelea na jitihada katika kuhakikisha upatikanaji wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa kahawa ikiendelea kushirikiana na Taasisi mbali mbali za kifedha zikiwemo za kilimo kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Taasisi ya kuwezesha masuala ya Kilimo (PASS), Benki ya Ushirika (COOP Bank Tanzania) na kadhalika, lengo likiwa ni kumuwezesha mkulima kupata mbolea kwa bei ya ruzuku na kulipa kwa riba nafuu baada ya mwaka mmoja.
Ameongeza kwa kusema lengo la Serikali ni kuongeza tija katika zao la kahawa kutoka tani 2.5-7.4 hadi kufikia tani 14 kwa hekari ambapo pamoja na suala la mbolea Seriakli pia imejipanga kuwezesha upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika zao hilo ,ikilenga kuvhimba visima katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya upatikanaji wa maji ya kutosha ikiwemo Songwe, Simiyu, Mbozi na kadhalika.
Katika hatua nyingine Bw. Primus amewahakikishia wadau hao kushirikiana na mrajisi wa vyama vya ushirika katika kushughulikia madeni chefu chefu katika vyama vya ushirika, ili kuwajengea wakulima imani na kudhibiti uuzaji holela na utoroshaji wa kahawa kutoka kwa wakulima, badala yake kahawa iuzwe kwa utaratibu uliowekwa.
Aidha, Serikali inaendelea na mpango maalumu ukishirikiana na Serikali za mikoa katika kuwatambua na kuweka rekodi ya wakulima wa zao la kahawa katika maeneo mbalimbali nchini, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za ugani na kudhibiti wizi na kumuwezesha mkulima kupata masoko ya uhakika ya zao la kahawa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa amesema lengo la Serikali ni kumuwezesha mkulima mdogo kunufaika na Sekta ya kilimo kupitia uzalishaji ambapo katika mkoa wa Kagera jumla ya hekari 4000 zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha kahawa kwa wakulima wadogo waliopo katika mkoa huo, huku lengo likiwa ni kupata eneo la hekari 10000 kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.
Tanzania inazalisha tani elfu 80 ya kahawa ambapo 46% inauzwa katika masoko ya Barani ulaya na nyingine ikiuzwa nchini Japan, Tanzania inazalisha kahawa aina ya Arabika katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga ,Iringa, Mbeya,Kigoma ,Mara, Manyara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Songwe na Katavi wakati kahawa aina ya Robusta ikilimwa Mkoani Kagera na Morogoro.
Tarehe 4 Julai, 2025
"TIJA KATIKA TASNIA YA KAHAWA NI KANUNI BORA ZA KILIMO"
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ( anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji) Dkt. Stephen Nindi amesema ili tija iweze kuongezeka katika Sekta ya kahawa ni lazima mkulima azingatie kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya pembejeo, upatikanaji wa huduma za ugani pamoja na miundombinu ya umwagiliaji katika kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji.
Dkt.Nindi ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Wadau wa Kahawa 2025 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper jijini Dodoma na kusema Wizara ya Kilimo itaendelea kuzalisha miche bora ya kahawa kwa kushirikaiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) kwajili ya wakulima, lengo likiwa ni kufikia miche milioni 100 kutoka miche milioni 20 inayozalishwa kila mwaka.
Wizara itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea katikaa kukidhi mahitaji ya mbolea ambayo ni tani 50,000 kwa mwaka, pamoja na kuimarisha huduma za ugani ambapo Sekta ya kahawa inahudumiwa na wagani rasmi 230 huku wasio rasmi wakiwa108.
Aidha, Dkt. Nindi ameitaka Bodi ya Kahawa nchini kuweka miundombinu ya uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua katika kukabiliana na ukame. Serikali inahakikisha upatikanaji wa masoko ya kahawa kupitia vyama vya ushirika ambavyo vimetakiwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania, Taasisi za Kifedha pamoja na Uongozi wa Halmshauri zote nchini katika kutoa elimu na kurudisha imani ya wakulima katika vyama vya ushirika.
Mkutano huu umehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya, Mkurugenzi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Bw. Thomasi Mbwana, Mkurugenzi Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania ( TOSCI), Bw.Enock Nyasebwa, Warajisi wa Vyama vya Ushirika, Wenyeviti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kahawa (Tanzania Coffee Association), Menejimenti ya Wizara ya Kilimo, Menejimenti ya Bodi ya Kahawa Tanzania, Watafiti wa Kilimo, Taasisi za kifedha, Mashirika binafsi, Wawakilishi wa wakulima wa kahawa kutoka katika Mikoa 17 inayolima kahawa nchini.