Imewekwa: 10 Sep, 2025
Uzinduzi wa Kahawa Festival 2025: Tanzania Kujitangaza Kimataifa Kupitia Kahawa

Tamasha kubwa la wadau wa kahawa nchini, maarufu kama Kahawa Festival 2025, limezinduliwa rasmi leo katika Makao Makuu ya Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro. Tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 Oktoba 2025, litawakutanisha wakulima, wasindikaji, wauzaji, wapenzi wa kahawa na watalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ambaye alipongeza juhudi za Bodi ya Kahawa Tanzania katika kuandaa tamasha hilo kwa lengo la kuinua sekta ya kahawa na kuipa nafasi Tanzania kwenye ramani ya kahawa duniani.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Bw. Primus Kimaryo, alisema tamasha hilo lina malengo makuu manane, yakiwemo kuhamasisha utalii na utamaduni wa unywaji wa kahawa nchini, kuongeza maarifa kwa vijana kupitia elimu ya kahawa, na kuonyesha ubora wa kahawa ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Kahawa yetu ni ya kipekee na yenye historia kubwa. Kupitia tamasha hili, tunataka kuongeza thamani ya kahawa kuanzia shambani hadi mezani, kutoa elimu kwa vijana na kufungua fursa za ajira katika mnyororo mzima wa thamani ya kahawa – kuanzia uchumaji, ukaangaji, usagaji, usafirishaji na biashara ya kimataifa,” alisema Kimaryo.

Aidha, alibainisha kuwa wageni wa kimataifa watapata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuchuma kahawa, kujifunza njia za kienyeji na za kisasa za ukaangaji, pamoja na kufurahia uzoefu wa utalii wa mazingira (eco-tourism) katika mashamba ya kahawa.

Kwa upande wake, Mhe. Babu aliwataka Watanzania kulinda mashamba ya kahawa kwa kuepuka tabia ya kukata miti ya zao hilo kwa matumizi binafsi.

“Turudi kwenye ramani ya kahawa duniani kwa kuongeza uzalishaji na ubora. Kahawa ndiyo chapa yetu kama taifa, hivyo tusipoteze fursa hii kwa kuharibu mashamba. Ni jukumu letu wote kuhakikisha tunalinda na kukuza zao hili la kimkakati,” alisema.

Tamasha hili linatarajiwa kuvutia maelfu ya wageni, wakiwemo wafanyabiashara wa kimataifa, wawekezaji, wapenzi wa kahawa na watalii, hivyo kuchangia kukuza uchumi wa ndani na kuongeza thamani ya zao la kahawa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.