Mkoa wa Ruvuma umeadhimisha Siku ya Kahawa Duniani kimkoa katika viwanja vya maonesho ya Kijiji cha Ngima,Kata ya Ngima, Wilaya ya Mbinga, kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa. Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI), Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na wadau wengine.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori.
Kwa mwaka huu, maadhimisho yameongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kura Yako Haki Yako, Shiriki Uchaguzi kwa Maendeleo ya Zao la Kahawa.”
Shughuli mbalimbali zilifanyika katika maonesho hayo ikiwemo unywaji wa kahawa, maonesho ya bidhaa mbalimbali zitokanazo na kahawa, pembejeo, mitambo ya kisasa ya kahawa, elimu juu ya kilimo bora cha kahawa, pamoja na utoaji wa zawadi kwa wabunifu wa bidhaa za kahawa ikiwemo bidhaa za urembo kama coffee scrub.
Akizungumza wakati wa kufunga maonesho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori, aliwapongeza waandaaji na wadau wote kwa kufanikisha tukio hilo. Pia aliwataka wakulima kuongeza uzalishaji wa kahawa kwa wingi zaidi ili kuchangia pato la taifa na kuinua uchumi wa kaya zao.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kufafanua dhana potofu kuwa unywaji wa kahawa unasababisha magonjwa kama shinikizo la damu na kisukari, akisisitiza kuwa dhana hiyo si ya kweli na kahawa ni kinywaji chenye faida nyingi kiafya na kiuchumi.

