Imewekwa: 11 Nov, 2025
MICHE 1,400,000 YA KAHAWA  YAGAIWA BURE KWA WANANCHI BUHIGWE

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Justin Ngayalina  ameongoza zoezi la ugawaji wa Miche takribani 1,400,000 bure kwa Wakulima wa kata ya Kibwigwa, Mwayaya na Mkatanga iliyozalishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma kupitia kampuni ya B - PLUS.


Akizungumza na Wananchi hao, Kanali Ngayalina amewasihi kuilea na kuitunza vizuri miche hiyo ili kupata mavuno yatakayo wakwamua kiuchumi kwa kila mkulima lakini pia kuiendeleza Nchi kupitia sekta ya kilimo.


Aidha ameipongeza  Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia Bodi ya Kahawa, Makampuni yanayojihusisha na kilimo na Wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Ndug George Emmanuel Mbilinyi kwa uamuzi wa kuzalisha miche hiyo katika maeneo ya Halmashauri.

 

Zoezi hili ni miongoni mwa mikakati ya Bodi ya Kahawa Tanzania  ya kuhakikisha ugawaji huu unachangia kuongeza tija na ubora wa zao la kahawa. Malengo ni kuhamasisha wakulima kupanda miche ya kisasa yenye uwezo wa kutoa mavuno makubwa, kuongeza mapato ya wakulima, na kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima, AMCOS na sekta binafsi.