Maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani kwa Kanda ya Mbeya na Songwe yamefanyika katika kiwanda cha MCC’Co wilayani Mbozi, mkoani Songwe mnamo tarehe 18 Novemba 2025, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabir Omar Makame.
Maadhimisho hayo yalikuwa chini ya kaulimbiu isemayo “Kutoka kwenye Ardhi ya Mtanzania Kwenda kwenye Kikombe cha Dunia.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Makame amewataka wakulima na wananchi kuzingatia kilimo rafiki kwa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikipunguza uzalishaji wa zao la kahawa nchini.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alieleza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), zikiwemo uanzishwaji wa visima na mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua kama chanzo kikuu cha maji ya kilimo.
Mhe. Makame aliongeza kuwa Serikali pia imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo bora cha kahawa, hatua ambayo inalenga kuongeza uzalishaji na kuongeza pato la Mkoa wa Songwe na Taifa kwa ujumla.
Akitoa takwimu za mafanikio ya mwaka huu, amesema kufikia Oktoba 2025 Mkoa wa Songwe umeingiza zaidi ya shilingi bilioni 52.4 kupitia mnada wa kahawa, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko mwaka uliotangulia.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wakulima ameishukuru Serikali kwa jitihada hizo, huku akiomba kuimarishwa zaidi kwa kilimo cha umwagiliaji kupitia TCB, ili kuongeza uzalishaji na tija kwa mkulima.

