Tamasha la Kahawa msimu wa sita kwa mwaka 2025 limehitimishwa kwa mafanikio makubwa baada ya kufanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Oktoba 3 hadi 5 katika kiwanda cha Tanganyika Coffee Curing Ltd, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Tamasha hilo ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa nchini na nje ya Tanzania, liliambatana na shughuli za maonesho ya bidhaa za kahawa, mashindano ya barista na cupping, mijadala ya kitaalamu pamoja na ziara za mafunzo kwa wakulima.
Akifungua rasmi tamasha hilo Oktoba 3, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Mheshimiwa Benson Ndiege, alitembelea mabanda ya maonesho na kueleza kufurahishwa na maandalizi yaliyofanyika. Alisisitiza umuhimu wa wadau wa sekta ya kahawa kuendelea kuwa wabunifu ili kuongeza tija na kukuza zaidi soko la ndani kupitia utamaduni wa unywaji wa kahawa nchini.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Mheshimiwa Raymond Mwangwala, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa siku ya kufunga tamasha hilo Oktoba 5. Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali, aliipongeza Bodi ya Kahawa Tanzania na waandaaji wa tamasha hilo kwa jitihada za kukuza tasnia ya kahawa na kutoa wito wa kuendeleza ushirikiano kati ya wakulima, wawekezaji na serikali katika kuongeza thamani ya zao hilo.
Tamasha la Kahawa limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza maarifa, ubunifu na uhamasishaji wa matumizi ya kahawa ya Tanzania, sambamba na kutangaza fursa za kibiashara kwa wakulima na wawekezaji.

