Imewekwa: 21 May, 2024
USAJILI WA MAKUBALIANO YA KILIMO CHA MKATABA

 

TANGAZO KWA UMMA

 

21 Mei, 2024

Moshi.

 

USAJILI WA MAKUBALIANO YA KILIMO CHA MKATABA

 

1.0 Utangulizi

Kwa mujibu wa kifungu 34 A (1) ya Sheria ya Tasnia ya Kahawa, 2001 kama ilivyorekebishwa mwaka 2009 pamoja na kanuni ya 59 (1) ya Kanuni za Tasnia ya Kahawa 2013, mkulima aliyesajiliwa anaweza, kwa madhumuni ya kuendeleza na kurahisisha shughuli za kilimo, kuingia mkataba wa kilimo na wafadhili, wanunuzi wa kahawa, wachakataji, wawekezaji au benki. Mifano ya shughuli za kilimo ni pamoja na upatikanaji wa pembejeo, utoaji wa huduma za ugani, usajili kwenye mifumo ya kahawa endelevu (certification) na usimamizi wa uendeshaji wa mitambo ya kuchakata kahawa.

Kwa mujibu wa kanuni ya 59 (2) ya Kanuni za Tasnia ya Kahawa 2013, mikataba wa kilimo itapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia rasimu iliyoainishwa katika Jedwali Na. 11 la Kanuni za Tasnia ya Kahawa, 2013 (Standard Form Agreement for Contract Farming). Mikataba yote ya kilimo itapaswa kuwasilishwa Bodi ya Kahawa Tanzania (Bodi) kwa ajili ya kupitiwa na kusajiliwa kwa mujibu wa kanuni ya 59 (3) ya Kanuni za Tasnia ya Kahawa, 2013. Mikataba yote ya kilimo itapaswa kupata idhini ya Ofisi ya Mrajisi wa Ushirika akiwa msimamizi wa vyama vya ushirika, kabla ya kuwasilishwa Bodi ya Kahawa kwa ajili ya mapitio na usajili.

Wakulima waliosajiliwa na watoa huduma wanaelekezwa kuzingatia na kutelekeza mambo yafuatayo katika utekelezaji wa sheria na kanuni hii;

1.1  Mtoa huduma atapaswa kuonyesha kwa uwazi katika mkataba wa kilimo gharama ambayo inatolewa kwa mkulima aliyesajiliwa au kwa Chama cha Msingi husika; kwa mfano, aina ya huduma, gharama kwa kilo, bei ya mbolea, riba zozote zitakazohusika na huduma ya uwezeshaji wa kifedha n.k.

1.2  Mkataba wa kilimo utakaowasilishwa Bodi kwa ajili ya usajili utapaswa kuambatana na nyaraka zifuatazo:-

1.2.1  Orodha ya wakulima waliosajiliwa au wanachama wanufaika wa chama cha msingi na ukubwa wa maeneo ya mashamba yao (individual acreage under coffee) pamoja na nyaraka za utambulisho (National Identification Cards).

1.2.2  Muhtasari wa mkutano wa chama cha ushirika ukionyesha uamuzi wa kuingia katika mkataba wa kilimo na mtoa huduma.

2.0  Kwa kuwa lengo la mikataba ya kilimo ni kuendeleza zao la kahawa, aina ya huduma za uwezeshaji zitapaswa kuendana na kalenda ya uzalishaji wa zao la kahawa katika eneo husika.

3.0  Mkulima aliyesajiliwa au Chama cha Msingi cha Ushirika aliyesajiliwa na kuingia katika mkataba wa kilimo atawajibika kurejesha gharama zote kwa mtoa huduma endapo atavunja masharti ya makubaliano na mtoa huduma.

4.0  Mikataba ya kilimo iainishe muda wa kuanza na kumalizika kwa majukumu ya pande zote mbili katika mkataba.

5.0  Mikataba ya kilimo ya usajili kwenye mifumo ya kahawa endelevu (certification) iwe na kifungu kinachoonyesha jinsi bei ya nyongeza (premium) itakavyolipwa na itakavyotumika.

5.1  Bodi itasimamia utekelezaji wa kila mkataba wa kilimo; aidha Bodi haitasajili mkataba wa kilimo wowote ambao utakiuka matakwa ya Sheria au Kanuni za Tasnia ya Kahawa.

6.0  Bodi inasisitiza kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria kwa mtoa huduma kutoa huduma ya aina yoyote kwa mkulima aliyesajiliwa bila kuwepo kwa mkataba wa kilimo uliosajiliwa na Bodi; kufanya hivyo itakuwa ni kinyume na kifungu namba 34 A. (5) na (6) cha Sheria ya Tasnia ya Kahawa, 2001 kama ilivyorekebishwa mwaka 2009.

 

Imetolewa na:

 

Primus O. Kimaryo

Mkurugenzi Mkuu

BODI YA KAHAWA TANZANIA

S. L. P. 732 – Moshi, Simu: 027-27-52324

Barua pepe: info@coffeeboard.go.tz; Tovuti: www.coffeeboard.or.tz