Imewekwa: 15 May, 2026
WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI TCB WAFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI KAGERA

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Aurelia K. N. Kamuzora, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Bw. Primus Kimaryo, leo tarehe 14 Mei 2026 wamefanya ziara ya kikazi mkoani Kagera kwa lengo la kujionea maendeleo ya sekta ya kahawa, kuimarisha usimamizi wa shughuli za uzalishaji pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na miche bora kwa wakulima wa kahawa nchini.

Katika ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walitembelea Kiwanda kikubwa cha Kahawa cha AMIMZA ambapo walipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uchakataji wa kahawa na hatua zinazochukuliwa katika kuongeza thamani ya zao hilo ili kuendelea kuinua ubora wa kahawa ya Tanzania na kuongeza ushindani wake katika soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha, wajumbe hao walitembelea kitalu kikubwa cha uzalishaji wa miche bora ya kahawa kilichopo Kijiji cha Ruanga, Kata ya Ruanga, Wilaya ya Muleba, ambapo walijionea juhudi zinazofanywa kuhakikisha wakulima wanapata miche bora yenye tija kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa zao la kahawa nchini.

Ziara hiyo pia iliwafikisha wajumbe katika shamba kubwa la vijana la Mradi wa BBT Makongora, ambapo walipata nafasi ya kujionea shughuli zote za uzalishaji shambani hapo pamoja na namna vijana wanavyoshiriki kikamilifu katika kilimo cha kahawa kupitia mifumo ya kisasa ya uzalishaji. Kupitia mradi huo, TCB inaendelea kuhamasisha ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo ili kuongeza ajira, uzalishaji na mchango wa sekta ya kahawa katika uchumi wa Taifa.

Ziara hiyo imeendelea kutoa nafasi kwa wajumbe wa Bodi kusikiliza mafanikio na changamoto zinazowakabili wadau wa sekta ya kahawa mkoani Kagera, sambamba na kuimarisha mikakati ya maendeleo ya zao hilo kuanzia ngazi ya uzalishaji, uchakataji hadi upatikanaji wa masoko yenye tija.

Bodi ya Kahawa Tanzania inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha sekta ya kahawa inakuwa endelevu, yenye ushindani na inayochangia kikamilifu katika kuongeza kipato cha wakulima na kukuza uchumi wa Taifa.