Imewekwa: 13 Oct, 2026
BODI YA KAHAWA TANZANIA YASHIRIKI JUKWAA LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA UMOJA WA ULAYA

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake, Bw. Primus Kimaryo, imeshiriki Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU–Tanzania Investment Roadshow) lililofanyika jijini The Hague, Uholanzi, tarehe 5–6 Oktoba 2026, kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.

Jukwaa hilo lilitoa fursa ya kutangaza sekta ya kahawa ya Tanzania kama eneo lenye fursa za uwekezaji, hususani katika kilimo, uchakataji na uongezaji thamani wa kahawa, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wawekezaji wa Ulaya katika kukuza ushindani wa kahawa ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Ushiriki wa TCB katika jukwaa hilo unaendana na juhudi za Serikali za kuvutia uwekezaji, kupanua masoko ya kahawa ya Tanzania na kuimarisha maendeleo endelevu ya mnyororo wa thamani wa zao hilo, kwa manufaa ya wakulima na wadau wengine wa sekta ya kahawa nchini.

Jukwaa hilo limefanyika kuelekea Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, linalotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwezi Februari 2027.