Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imeibuka mshindi wa nafasi ya tatu katika kundi la Bodi za Kilimo na Mifugo zilizofanya vizuri kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane) 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malechela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Aidha, Bodi ya Kahawa Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) iliibuka mshindi wa kwanza katika kundi hilo katika maonesho ya Nanenane yaliyofanyika katika ngazi ya kanda, hatua inayoakisi ubora wa huduma, elimu na juhudi za kuhamasisha maendeleo ya sekta ya kahawa zinazotolewa na TCB nchini.
Tuzo hiyo ya kitaifa ilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni utambuzi wa mchango wa TCB katika kutoa elimu kwa umma, kuhamasisha maendeleo ya sekta ya kahawa na kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau waliotembelea banda la Bodi hiyo wakati wa maonesho.
Mafanikio hayo yanadhihirisha dhamira ya Bodi ya Kahawa Tanzania ya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma, kuhamasisha uzalishaji wa kahawa wenye tija na kuendeleza sekta ya kahawa nchini kupitia elimu, ubunifu na ushirikiano na wadau mbalimbali.

