Imewekwa: 23 Feb, 2026
KAMPENI MAALUM YA KUHAMASISHA UNYWAJI WA KAHAWA YA NDANI

Idara ya Ubora na Uhamasishaji ya Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imezindua rasmi kampeni maalum ya kuhamasisha unywaji wa kahawa ya ndani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa TCB kuongeza matumizi ya kahawa ya ndani hadi kufikia asilimia 15 ya kahawa yote inayozalishwa hapa nchini.

Kampeni hiyo kwa sasa inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma, ambapo wananchi, na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa wanapatiwa elimu kuhusu faida za kiafya na kiuchumi za zao la kahawa pamoja na umuhimu wa kuunga mkono matumizi ya bidhaa za ndani. Zoezi hili linatarajiwa kuendelea katika mikoa mingine nchini ili kuhakikisha linawafikia Watanzania wengi zaidi.

Sambamba na utoaji wa elimu, TCB inatekeleza zoezi la utambulisho na uuzaji wa bidhaa bora za kahawa zinazozalishwa nchini, ikiwemo kahawa chapa ya Tancafe inayozalishwa na Bodi ya Kahawa. Wananchi wanapata fursa ya kuonja na kununua kahawa hiyo moja kwa moja, hatua inayolenga kuimarisha soko la ndani, kuongeza thamani ya zao la kahawa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kupitia kampeni hii, TCB inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kukuza utamaduni wa unywaji kahawa nchini na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama mzalishaji wa kahawa bora duniani. Wananchi wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hili na kuunga mkono juhudi za kukuza soko la ndani la kahawa.