Imewekwa: 07 May, 2026
KONGAMANO LA PILI LA WAKAANGAJI WA KAHAWA LAFANYIKA MOSHI

Kongamano la Pili la Wakaangaji wa Kahawa kwa mwaka 2025/2026 lililofanyika  Mei 06, 2026, Makao Makuu ya Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro, limewakutanisha kwa Pamoja wakaangaji wa kahawa  kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili masuala muhimu ya kuendeleza sekta hiyo.

Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha wadau hawa muhimu katika sekta ya kahawa kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili, kubadilishana uzoefu, kupata elimu pamoja na kutambua na kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo. Aidha, kongamano hilo lilitoa jukwaa la wadau hao kufikia maazimio yatakayowawezesha kuwa na sauti moja katika kuendeleza sekta ya kahawa nchini.

Akifungua kongamano hilo, Mgeni Rasmi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Bw. Primus Kimaryo, aliwataka wakaangaji wa kahawa kutambua nafasi yao muhimu katika kukuza matumizi ya kahawa ndani ya nchi.

Aidha, aliwahimiza wakaangaji kushiriki kikamilifu katika maonesho ya ndani na kimataifa ili kuitangaza zaidi kahawa ya Tanzania na kuongeza ushindani wake katika soko la dunia.

Katika kongamano hilo, washiriki walipata mafunzo na elimu mbalimbali kutoka kwa taasisi zilizoshiriki, zikiwemo Mfuko wa Udhamini wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Taasisi hizo zilitoa elimu kuhusu fursa zilizopo, uzingatiaji wa viwango, pamoja na masuala ya uhifadhi wa mazingira katika shughuli za ukaangaji wa kahawa.

Kwa upande wao, wakaangaji wa kahawa walijipongeza kwa ongezeko kubwa la wanachama waliojisajili na kutambulika rasmi na Bodi ya Kahawa Tanzania, hatua ambayo imeongeza uhalali na ushindani wao katika soko. Aidha, waliwasihi wale ambao bado hawajajisajili kufanya hivyo ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali na wadau wa sekta hiyo.

Kongamano hili ni sehemu ya juhudi za Bodi ya Kahawa Tanzania katika kuimarisha sekta ya kahawa nchini kwa kuwajengea uwezo wadau wake na kukuza matumizi ya kahawa ya ndani pamoja na masoko ya kimataifa.