Mkutano mkuu wa 16 wa Mwaka wa Wadau wa Kahawa nchini umehitimishwa kwa mafanikio makubwa baada ya kufanyika kwa siku mbili, Juni 4 na 5, 2026 katika Ukumbi wa Vincent, St. Gaspar Hotel and Conference Centre mjini Dodoma.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge,wakurugenzi wa halmashauri, vyama vya ushirika, wakulima, wafanyabiashara wa kahawa pamoja na taasisi za Serikali na sekta binafsi kwa lengo la kujadili maendeleo ya sekta hiyo na kufikia maadhimio yatakayochochea ukuaji wake.
Akifunga mkutano huo, Mgeni rasmi wa mkutano huo Waziri wa Kilimo, Mhe.Daniel Chongolo(MB), aliagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa na wilaya kuhakikisha wanunuzi wote wenye madeni kwa wakulima hawaruhusiwi kushiriki ununuzi katika msimu ujao, huku akisisitiza kuwa Serikali haitatoa leseni kwa mnunuzi yeyote ambaye hajalipa madeni hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya kahawa Bw. Primus Kimaryo alisema mkutano huo umejadili mafanikio, changamoto na fursa za sekta ya kahawa pamoja na kuweka mikakati ya kuendelea kuboresha uzalishaji, biashara na masoko ya zao hilo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya kahawa Profesa Kamuzora alisema ushiriki mkubwa wa wadau na maadhimio yaliyofikiwa yanaonesha dhamira ya pamoja ya kuendelea kuimarisha sekta ya kahawa, huku akiipongeza Bodi ya Kahawa Tanzania kwa kuendelea kuratibu juhudi za maendeleo ya zao hilo nchini.

