Imewekwa: 16 Oct, 2026
TANZANIA YAENDELEA KUTANGAZA KAHAWA YAKE KATIKA MAONESHO YA SCAJ 2026 NCHINI JAPANI

Wizara ya Kilimo,kupitia Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), kwa kushirikiana na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Japani, inaendelea kutangaza kahawa ya Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Maalumu (SCAJ 2026), yanayofanyika nchini Japani kuanzia tarehe 14 hadi 17 Oktoba 2026.

Ushiriki huo unalenga kutangaza kahawa za Tanzania aina ya Arabika na Robusta, kupanua masoko ya kimataifa na kuimarisha uhusiano wa kibiashara na wadau wa sekta ya kahawa.

Katika maonesho hayo, TCB imewezesha ushiriki wa kampuni tano za kahawa ambazo ni Karagwe Estates Limited, Megnacio Company Limited, Lutefo Coffee Farm Limited, DRK General Merchants Ltd na Skyline Winner Company Ltd. Kampuni hizo zimepata fursa ya kufanya mazungumzo ya kibiashara na kampuni mbalimbali za Japani, zikiwemo Ueshima Coffee Company Limited (UCC), Tully’s Coffee, Key Coffee Roasting Company, S. Ishimitsu & Company Limited na Marubeni Corporation, kwa lengo la kutafuta wanunuzi wapya na kufungua fursa zaidi za biashara.

Aidha, wageni waliotembelea banda la Tanzania wamepata fursa ya kuonja kahawa ya Tanzania, inayojulikana pia katika soko la Japani kama Kilimanjaro Coffee, na kutoa maoni chanya kuhusu ubora na ladha yake.

Ushiriki wa Tanzania katika SCAJ 2026 ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza ushindani wa kahawa ya Tanzania katika soko la kimataifa, kupanua masoko ya nje na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Japani.

Pichani: Balozi wa Tanzania nchini Japani, Mhe. Anderson Mutatembwa, akiwa pamoja na wawakilishi wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Bw. Rogatus Meela na Bi. Naishoki Lucumay, maafisa wa Ubalozi na wawakilishi wa kampuni zilizoshiriki katika Maonesho ya SCAJ 2026.