Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Bw.Primus Kimaryo, ashiriki katika mdahalo wa kimataifa kuhusu mustakabali wa sekta ya kahawa barani Afrika, uliofanyika tarehe 25 Agosti 2026 katika Meeting di Rimini, Italia.
Mdahalo huo uliokuwa na mada “Chicchi di caffè in Africa. Giovani e formazione per filiere sostenibili” wenye maana ya “Kahawa Barani Afrika:Vijana na Mafunzo kwa Minyororo ya Thamani Endelevu” ulijikita katika nafasi ya vijana, mafunzo na ujenzi wa mnyororo wa thamani wa kahawa unaozingatia uendelevu.
Katika mdahalo huo, Bw.Kimaryo alishiriki pamoja na viongozi na wataalamu kutoka nchi mbalimbali zinazozalisha kahawa barani Afrika, akiwemo Adugna Debela, Mkurugenzi Mkuu wa Ethiopian Coffee and Tea Authority kutoka Ethiopia, Henry Kinyua kutoka Kenya, pamoja na Chiara Scaraggi, mtaalamu wa Coffee Value Chain kutoka UNIDO. Pia walishiriki wawakilishi kutoka sekta ya kahawa nchini Italia na taasisi za maendeleo.
Mdahalo huo pia ulihusisha uwepo wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, ambaye alihudhuria Meeting di Rimini na kuwa miongoni mwa viongozi wakuu waliokuwepo katika mkutano huo wa kimataifa.
Katika mchango wake, Bw. Kimaryo alieleza hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuendeleza sekta ya kahawa, ikiwemo kuongeza uzalishaji, kuwahusisha vijana na kuimarisha ujuzi katika mnyororo wa thamani wa kahawa.
Ushiriki wa Bw. Kimaryo katika mdahalo huo unaendelea kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika mijadala ya kimataifa inayolenga maendeleo ya vijana, mafunzo, uendelevu na kuongeza thamani na ushindani wa kahawa ya Afrika katika masoko ya dunia.

