Imewekwa: 24 Aug, 2026
TCB, ITC WAIMARISHA UWEZO WA WATAALAMU KATIKA UBORA NA BIASHARA YA KAHAWA GHAFI

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) kupitia programu ya MARKUP II, imeendesha mafunzo ya SCA Green Coffee Foundation na Intermediate kwa vijana 42, kuanzia tarehe 17 hadi 22 Agosti 2026, yakilenga kuimarisha ujuzi wao katika ubora na biashara ya kahawa ghafi.

Mafunzo hayo yalijikita katika kuwawezesha vijana hao kutambua, kutathmini na kueleza sifa za kahawa kutoka maeneo mbalimbali nchini, pamoja na kupata ujuzi kuhusu uchakataji, upangaji wa madaraja, uchambuzi wa sampuli, unyevu,uhifadhi na mnyororo wa ugavi.

Aidha, washiriki walipatiwa uelewa kuhusu mahitaji ya masoko na misingi ya biashara ya kahawa ghafi, hatua inayolenga kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika sekta ya kahawa na kuongeza uwezo wa sekta katika kudhibiti ubora, kuongeza thamani na kuwasilisha kahawa ya Tanzania kwa ufanisi zaidi katika masoko ya ndani na kimataifa.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za TCB na ITC kupitia MARKUP II za kujenga uwezo wa vijana katika mnyororo wa thamani wa kahawa, kuimarisha ushindani wa kahawa ya Tanzania na kuongeza fursa za ajira na biashara katika sekta hiyo.