Imewekwa: 03 Mar, 2026
TCB KUGAWA MICHE MILIONI 20 BURE YA RUZUKU KWA WAKULIMA NCHINI

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais  Samia Suluhu Hassan unaendelea kuimarisha sekta ya kahawa nchini kupitia zoezi la ugawaji wa miche ya kahawa ya ruzuku bure kwa wakulima katika kanda zote za uzalishaji.

Zoezi hilo linaratibiwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), ambapo jumla ya miche zaidi ya milioni 20 inagawiwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali yanayozalisha zao la kahawa nchini. Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza uzalishaji, kuinua tija mashambani na kuboresha ubora wa kahawa ya Tanzania ili iweze kushindana katika soko la ndani na kimataifa.

Kwa mujibu wa TCB, ugawaji huo unalenga pia kupanua mashamba ya kahawa kwa kuwafikia wakulima wapya na kuimarisha mashamba yaliyopo, sambamba na kuwahamasisha wakulima kutumia miche bora yenye tija na inayostahimili magonjwa.

Zoezi hilo linaloendelea katika kanda zote za uzalishaji linaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima, kuongeza kipato chao na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia zao la kahawa.

Kupitia usimamizi na uratibu wa TCB, serikali imejipanga kuhakikisha miche hiyo inawafikia walengwa kwa wakati na kwa usawa, ikiwa ni hatua muhimu katika kuleta mapinduzi chanya ya kilimo cha kahawa nchini.