Imewekwa: 31 Jul, 2026
TCB YAPOKEA UGENI KUTOKA DRC KUJIFUNZA MAFANIKIO YA SEKTA YA KAHAWA TANZANIA

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imepokea ugeni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mazao ya Kilimo ya Kongo (Office National des Produits Agricoles du Congo – ONAPAC), Bi. Mimy Monga Numbi, uliowasili nchini kujifunza uzoefu wa Tanzania katika maendeleo na usimamizi wa sekta ya kahawa.

Wakati wa ziara hiyo, ugeni huo ulipata fursa ya kujifunza kuhusu mfumo wa usimamizi wa sekta ya kahawa nchini unaoratibiwa na TCB, ukiwemo uzalishaji, udhibiti wa ubora, biashara na masoko, pamoja na mikakati mbalimbali inayotekelezwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa kahawa na kuimarisha mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa.

Aidha, ugeni huo ulitembelea Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), ambapo ulijionea shughuli za utafiti na ubunifu zinazotekelezwa ili kuendeleza zao la kahawa kupitia shughuli za uzalishaji wa miche bora, udhibiti wa magonjwa na wadudu, pamoja na teknolojia zinazolenga kuongeza tija na ubora wa kahawa nchini.