Imewekwa: 20 Jul, 2026
TCB Yashiriki Jukwaa la Biashara Tanzania na Misri.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Bw. Primus Kimaryo, pamoja na viongozi wengine wa sekta ya kilimo, washiriki Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Misri linalofanyika tarehe 18 Julai 2026 katika Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi nchini Tanzania.

Jukwaa hilo linanyika baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumpokea mgeni wake, Rais Abdel Fattah El-Sisi, Ikulu jijini Dar es Salaam. Likiwakutanisha viongozi wa serikali, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Misri kwa lengo la kujadili na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo, uwekezaji, afya, maji, nishati, elimu na miundombinu.

Kwa upande wa sekta ya kahawa, ushiriki wa Bodi ya Kahawa Tanzania katika jukwaa hilo unafungua fursa za kutangaza kahawa ya Tanzania na kuimarisha mahusiano ya kibiashara na soko la Misri, ambalo ni miongoni mwa masoko muhimu ya kahawa barani Afrika, likiwa na matumizi ya takribani tani 63,000 za kahawa kwa mwaka. Kupitia ushirikiano huu, Tanzania inalenga kuongeza fursa za biashara na masoko mapya kwa kahawa yake, sambamba na kukuza thamani ya zao hilo katika soko la kimataifa.