Imewekwa: 14 Jul, 2026
TCB Yatwaa Tuzo Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imetunukiwa tuzo baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi la waoneshaji wa Bidhaa za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla ya kufunga rasmi Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba yaliyofanyika tarehe 13 Julai 2026, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alikuwa mgeni rasmi. Katika hafla hiyo, washiriki mbalimbali walitambuliwa na kutunukiwa kwa umahiri wao katika kushiriki na kuonesha bidhaa na huduma zilizochangia mafanikio ya maonesho hayo.

Ushindi huo unadhihirisha mafanikio ya Bodi katika kutangaza ubora wa kahawa ya Tanzania, kutoa elimu kuhusu sekta ya kahawa na fursa za uwekezaji, pamoja na kuwafikia maelfu ya wananchi na wadau waliotembelea banda lake katika kipindi chote cha maonesho. Tuzo hiyo ni chachu ya kuendelea kuimarisha juhudi za kukuza uzalishaji, kuongeza thamani na kupanua masoko ya kahawa ya Tanzania ndani na nje ya nchi.