Imewekwa: 24 Jul, 2026
UGENI KUTOKA PAPUA NEW GUINEA WATEMBELEA TCB KUJIFUNZA MAFANIKIO YA SEKTA YA KAHAWA TANZANIA

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imepokea ugeni wa wadau wa sekta ya kahawa kutoka Papua New Guinea kwa lengo la kujifunza mafanikio, uzoefu na mbinu zinazochangia maendeleo ya sekta ya kahawa nchini Tanzania.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Bw. Primus Kimaryo, aliuelezea ugeni huo maendeleo ya sekta ya kahawa nchini, akifafanua mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo kuanzia uzalishaji, utafiti, ugani, usindikaji, biashara, masoko pamoja na mikakati ya kuongeza tija, ubora na thamani ya kahawa ili kuinua kipato cha wakulima na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.

Ugeni huo pia ulitembelea Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) kujifunza kuhusu tafiti na ubunifu unaofanyika katika kuboresha uzalishaji wa kahawa, kabla ya kutembelea shamba la kahawa la Kilimanjaro Plantations Limited (KPL) pamoja na baadhi ya wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro ili kujionea kwa vitendo matumizi ya teknolojia na mbinu bora za kisasa za uzalishaji.

Ziara hiyo imelenga kutoa fursa kwa wadau hao wa sekta ya kahawa kutoka Papua New Guinea kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya kahawa, hususan katika kuongeza uzalishaji, thamani ya zao na ushindani wake katika masoko ya kimataifa.

Aidha, ziara hiyo inaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Papua New Guinea katika sekta ya kahawa kupitia kubadilishana uzoefu, maarifa, teknolojia na mbinu bora za uzalishaji, huku ikiendelea kuithibitisha Tanzania kama moja ya nchi zinazotoa mfano wa mafanikio katika maendeleo ya sekta ya kahawa.