Imewekwa: 02 Apr, 2026
WAKULIMA WA KAHAWA KUGAWIWA MICHE YA KAHAWA MKOANI KILIMANJARO

Serikali kupitia Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati katika kuimarisha sekta ya kahawa na kuinua uchumi wa wakulima kwa kuzindua zoezi la ugawaji wa miche zaidi ya laki tano ya kahawa bure kwa wakulima wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza katika uzinduzi wa zoezi hilo lililofanyika tarehe 30 Machi 2026 katika Kijiji cha Kiruweni, Kata ya Mwika Kusini, Jimbo la Vunjo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Hassan Babu, aliipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuendeleza zao la kahawa, akieleza kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa huo. Aidha, aliwataka wakulima kuacha mara moja tabia ya kukata miti ya kahawa na badala yake kuendeleza mashamba yao ili kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Babu pia aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia sekta ya kilimo cha kahawa, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuhakikisha zao hilo linaendelea kuwa nembo ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Bw. Primus Kimaryo, alieleza kuwa ugawaji wa miche hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini na kuboresha kipato cha wakulima. Aliwataka wakulima kuhakikisha wanapanda miche wanayoipokea ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria katika kuwawezesha wakulima na kukuza zao hilo la kimkakati.

Zoezi hili linatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wakulima wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wananchi, na kufungua ajira zaidi hususan kwa vijana. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta ya kahawa inazidi kukua na kuwa na tija kwa taifa.